Kule Nako Poem by Fadhy Mtanga

Kule Nako

Labda kichwa chauma,
Njaa zaidi ya homa,
Kama vile unalima,
Pale moto unapochoma,
Na pia huwezi sema.

Wadhani ipo hekima,
Ndivyo ulivyozisoma,
Nyakti ukazipima,
Ni kwa baya ama jema,
Ulijuwe la kusema.

Ishara za wao wema,
Majini zinapozama,
Ukahitaji egema,
Ukidhani usalama,
Na ndivyo ulivyosema.

Imani haitogoma,
Ilikwambia mapema,
Punguzo la yako homa,
Ongezeko la naima,
Hata watu walisema.

Tumaini linazima,
Ugunduapo si pema,
Wao wanakuandama,
Kwa chuki na si huruma,
Kwa mabaya kukusema.

Watakutaka kuzama,
Hawishi kukusakama,
Ushindwe mbele tazama,
Malengo yako kugoma,
Halafu wanakusema.

Watakupa na tuhuma,
Upatwe nayo zahama,
Ushindapo yawauma,
Wanaanza kulalama,
Wanazidi tu kusema.

Kwa uimara simama,
Tazama mbele daima,
Kamwe usirudi nyuma,
Kuwa na moyo wa chuma,
Watashindwa la kusema.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success