Muhogo Mtamu. Poem by Abdallah Mpogole

Muhogo Mtamu.

1.Tule muhogo jamani, chakula cha wananchi.
Wala tusione soni, tafuna ilo mibichi.
Ifuateni sokoni, hamsini tu jisachi.
Chakula cha watu wote, yupi asema ukata?


2.Wakulima jitumeni, muwalishe wa mijini.
Machweo u’ kaangoni, watu haweshi foleni.
Yajaza mate kinywani, kwa chachandu ndo nyumbani.
Waloidharau dume, watafuna kwa aibu.


3.Muhogo acheni nyie! Mlo wa watu wa kale.
Magandaye ubandue, chemsha mtoto ale.
Weak pahala upowe, uchambue kwa upole.
Ipo dhana ya ufukara, sintoiacha asili.

4.Mwanzo nalidhani kweli, kripsi si muhogo.
Kumbe duara pingili, vifuko vidogovidogo.
Meno yapata shughuli, ati aponda muhogo.
Nimewaona kwa macho, wakimung’unya vigogo.

5.Naketi kwetu bandani, zogo limejaa tele.
Juma ataka sahani, jasho zamtoka Sele.
Twala muhogo jamani, sina hamu ya mchele.
Acheni kutushangaa, ingia mwone uhondo.


6.Rangi yake ni nyeupe, japo wachimbwa topeni.
Unga wake ukauke, Ugali wake ni shani.
Walo wagonjwa wapike, iwe afya mwilini.
Muhogo hana maringo, aishi palo ukame.


7.Ramadhani ndo futari, shuleni wana wakena.
Palo dhiki yasitiri, wanunuzi wang’ang’ana.
Masikini kwa tajiri, muhogo kwao dhamana.
Aina yake ni wanga, nguvu na joto mupate.


8.Tamatini napepea, utamu wanizidia.
Sintoacha kutetea, nitajaza sufuria.
Watasema ni kufulia, sijayaona madhila.
Waungwana jilieni, muhogo chakula bora.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success