Kwani Vipi? Poem by Fadhy Mtanga

Kwani Vipi?

Maneno yake mtu yule,
Alipokutana nao watu wale
Mahala palepale ambako hutokea,
Wangekutana hata na zaidi
Kwa sababu hutokea kuwa hivyo,
Ndipo mtu yule,
Alipoanza gumzo lake.

“Kwani vipi? ”
Vipi kitu gani, cha nini?
Ndiyo maswali yaake hayo
Na majibu yake je?
Utanijibia weye.

Mwingine kajibu, “sijui! ”
Mie nikamshangaa sana
Kwani ni nini asichokijua?
Hata akatae kutowa jibu
Linaloeleweka.

Wote wakajiuliza
Wengine mara mbili mbili
“Kwani ni vipi? ”
“Heeh! ” Wote wanashangaa.

Mmoja akanigeukia mimi
“Wafahamu weye? ” kauliza
Nafahamu nini?
Pengine jina lake!
Kwangu ni la nini sasa?
Si’ ndiyo hapo!

Visa? Mikasa? Hadithi je?
Yalitukia hayo mambo
Lini hasa? Labda jana
Hapana, ni miaka mingi
Alaa kumbe!



Sikuwapa jibu mie
Walilolitaka wao
Ningewajibu nini?
Kwani wameuliza nini?
“Heeh! Kumbe hujui! ”

Wala!
Nikawaambia wao
Wao wale wale
Niliokuwa nao.

Yafungueni macho yenu
Yaitazame dunia
“Kuna nini kwani? ”
Yakiona yatasema
Kweli yatasema.

Mie ninaogopa sana
Hata nani mwingine?
Anayeogopa?
Kwanini basi aogope?
Kwani anaogopa nini?
Wote wakakosa jibu.

“Hatukuelewi, tufafanulie”
Wote wakaniambia
Nikacheka chini chini
Hawa nao!

Nikawaambia,
Kama nyie hamuwezi sema
Mimi ndiyo kabisa
Nigeieni basi ujasiri
Kuyahimili hayo machungu.

“Ya nini kwani? ”
Eti wakaniuliza
“Kwani nawe umetazama nje? ”
Wakaniuliza swali
Wajue nimeona nini.

Mara wakamwona nyoka
Yu mwenye akili nyingi
Atambaa kwa tumbole
Ajipinda hapa na pale.

Anazungusha machoye
Ajipinda kugonga kokote
Akijilinda kiakili
Aulinda na mwiliwe
Kumbe yupo makini!

Japo anaweza
Hapeleki kichwa mkiani
Ati, akajing’ata mwenyewe
Kwa sababu yu ajua
Tena anajua vema.

Maumivu yake yale
Yatampata mwenyewe
Mwenyewe kabisa
Mbona angejiju!

Basi, kumbe yu mwerevu
Ndiye alompa tunda Eva
Na mumewe wakategeka
Wakajinoma na tunda
Tunda, tunda, tunda.
Acha kabisa!

Walipomaizi hilaye
Kajibu, “mi simo kabisa
Tamaa yenu imewaponza”
Wakajiju wao wenyewe
Mbona sana.

“Tumechoka hatukuelewi”
Wenzangu wakasema
Kwani nyie nyoka hamjamwona?
Ikanibidi kuwauliza.

“Tumemwona bwana
Tuambie sasa, ahusika vipi? ”
Nami nikawageukia
Kwani vipi?
Wakasema hawanielewi
Wana vichwa vigumu hao!
Kweli kabisa.




Mchuma janga?
Wote kwa pamoja wakajibu
“Hula na wa kwao! ”
Kumbe mnajua.

Wakanitazama, wakasema
“Mbona waongea sana?
Umemzungumzia nyoka
Mara mchuma janga
Mbona havihusiani? ”
Wakaniuliza bwana.

Mara eropleni ikapita
Ileee juu angani
Mwaiona hiyo?
Wote wakaangalia juu
“Tumeiona! ”

“Wewe bwana wewe
Hebu wacha mambo yako
Eropleni nayo pia?
Wataka tu unda visa”
Wakanishutumu.

Nataka mtu anieleze
Nikawaambia wao
Kama mtu kawahi kuiona
Eti yarudi rivasi
Iwapo angani?

Wakahadaika kwa sana
Kumbe hawakuwahi fikiri hilo
Hata siku moja ile!
Soni ikawajaa
Wakaangalia chini.

Mmoja wao akajibu
“La hasha swahiba!
Hata siku moja
Mie sijawahi kuiona”

Wenzake wakatahayari
Kaupata wapi huo ujasiri
Na akili yenye kufikiri
Kama mwanazuoni
Aliyekomaa.
Waungwana wangu nyie
Nyoka yupo wapi tena?
“Amekwisha potelea mbali”
Eti wakanijibu
Nikaishia kukenua meno.

Eropleni nayo?
“Imepotelea mawinguni”
Lini tutaitafuta basi?
“Heeh! Kuitafuta kivipi? ”
Wanazuga hawajanielewa.

Iiteni basi
Irudi hadi pale ilipokuwa
Nikawaagiza wao
Wakaishia kubabaika.

“Mwenyewe umeshasema
Eropleni hairudi rivasi”
Wakahitimisha wao
Kana kwamba nilisema
Wakanishangaza sana.

Ikanibidi kuwaambia
Sikusema hivyo jama
Ila niliwauliza swali
Kama mtu alikwishaiona
Eropleni ikirudi rivasi.

Wakaangaliana kwa zamu
Kuukiri huo ujinga wao
Wa kushindwa kunielewa
Hebu nisaidie wewe
Ni mimi niliyesema?

Najua utajibu ‘hapana’
Ukiamini sikusema mimi
Lakini ni nani aliyezua hoja?
Usisumbuke tena kunijibu.

Imeshakwenda jama
Ni kama muda, haitorudi nyuma
Hata kama itapita hapa tena
Itakuwa ni tarehe nyingine
Ama sijaeleweka?
Nipo tayari kufafanua.

Kabla hata sijawajibu
Wote tukaugundua
Mto uliopita pembeni
Upelekao maji baharini.

Mbona huo hamuushangai?
Nikawagonga kwa swali
“Hatuushangai kivipi? ”
Wakazidogodesha fikra zao
Kuniuliza tena mimi.

Mto wapeleka kila siku
Majiye upande mmoja
Na kamwe haitokei
Kuyarudisha maji yale
Kule yatokako.

Labda niwaulize swali
Nikawaambia wao
“We’ bwana uliza tu!
Maana waona raha sana
Kutupa sie karaha
Kwa maswaliyo tata.”

Nani ashawahi kuyavuka
Maji ya mto
Mara mbili?
Wote wakaitikia kwa nguvu
Kwamba wamewahi.

Msiwe wapumbavu nyie
Na wavivu wa kufikiri
Hakuna awezaye
Hata siku moja
Kuyavuka maji ya mto
Mara mbili.

Wakingali kushangaa
Nikazidi wapasulia
Mbona watakoma
Nimewapania sana leo.

Enyi mambumbumbu
Maji yale ya mto
Huja na kupita
Na kila unapovuka
Unavuka maji mapya.

Wakastaajabia sana
Maneno yanitokayo
Hawakuwa wamefikiria
Jambi hilo kabla
Na kweli!
Mmoja wao akainuka
Akiwa amefura hasira
Tena akanikwida
Ilhali yu na ngumiye mkononi.

“We baradhuli! ”
Akaniita mie hivyo
“Waona raha kutughilibu
Tena pia kutunanga
Umechonga sana
Ukitufanya sote mafala.”

Nikapata ujasiri
Nikawagonga wote kwa swali
Ati, kuna mtu amenisikia
Nikiwaita kwa jina hilo?
Asiogope basi aseme.

Nilipoona hawanijibu
Nikaendelea kuwaambia
Siku zote macho hutazama
Wakanijibu, “sawa.”

Na masikio husikia
Wakadakia, “ni kweli’
Jamaa yangu akashusha mkono
Sijui kaogopa kitu gani
Yu mwoga kama kunguru
Haki ya Mungu!

Nikasema tena
Lakini si fikra mgando
Ziwazo daima sahihi
Katika kuamua
Iwe hasi ama chanya.

“Mmhh! Wote wakaguna
Hawakuambulia lolote
Nami nikalitambua hilo
Nikawasikitikia sana
Sana tu!

Najua hamjanielewa
“Nani hajakuelewa?
Siye tumeelewa zaidi yako
Usijione kama mwerevu sana
We’ si lolote, si chochote”
Wakasema wao.

“Kwani vipi?
We’ ndiyo nani hasa
Hata ukatucheza shere
Kwa maneno yako ya shombo? ”

“Tatizo lako wewe
Wajifanya wajua sana
Hakuna chochote ukijuacho
Zaidi ni ushamba tu.”

Yamekuwa hayo tena
Ikanibidi kuwashangaa
Mbona mie sijadhamiria
Kumaliza kwa ugomvi
‘Kama nimewakwaza
Basi nisameheni.’

Hapo ndipo wakakenua
Kujitia zaidi ugangwe
Laiti kama wangejua
Hata wasingethubutu.

Naomba pia niseme
Wakatulia kunisikiliza
Jamani kukiri udhaifu
Wala hakumdhoofishi mtu
Bali
Kunamuimarisha.

“Ki vipi? ”
Mmoja akabwatuka
Nikaamua kutomjibu
Kadri ya anavyotaka
Sikuona haja
Sentensi yajieleza vema.

Kwa nini hamnielewi?
Ilhali lugha ni nyepesi mno
Swali langu hilo kwao
Likakosa jawabu.

“Bwana mkubwa weye”
Mwanamke akaniambia
“Huna jipya kabisa
Nahisi watupotezea muda
Ni heri utuwache
Tuendelee na mambo yetu.”

Mwingine naye akadakia
Kana kwamba hakuwepo awali
“Ni kweli uyasemayo
Huyu bwana hana sababu
Ya kutuwekesha siye hapa
Kwa ngonjera zake
Zisizo na mantiki kabisa.”

Halafu tena akanisonya
Hasira zikataka kunipanda
Lakini haikuwa hivyo.

Nikawaambia,
Yeyote hufanya jambo
Akiwa na yake sababu
Liwe zuri ama baya
Hujua alifanyalo.

Na kwamba akosaye sababu
Hufananishwa na kuku
Akazanae kudonoa
Hata asipokijua
Kitu akidonoacho.

Si maneno yangu hayo
Wala tusitakiane ubaya
Bali ni wao wenye hekima
Wale wajuvi wa maarifa
Wafanyao bidii kufikiri
Ndiyo wamesema hivi.



Nikawaona wote kimya
Nikaelewa sasa wamechoka
Nimepiga gumzo muda mrefu
Na bado hawajanielewa hata.

Lakini mmojawao akainuka
Akaongea kwa kunong’ona
“Aibu yetu sasa i wazi
Ni kama mfalme aliye uchi.”

“Manenoyo madini
Na wapumbavu hawatakuelewa
Kwa sababu wanaona uvivu
Kufikiri kwa juhudi
Ili waweze kuing’amua
Nguvu ya maneno yako.”

Nikawaambia sasa
Kwa kawaida huwezi kutambua
Kuwa umelala
Hadi pale,
Wakadakia wenyewe
“Utakapoamka! ”
Unadhani mimi sasa,
Ningesema neno gani tena?

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success