KAPCHANGA MARK KWEMOI

Rookie (22.02.1983 / Kitale, Kenya)

Majanga Yatumaliza - Poem by KAPCHANGA MARK KWEMOI

Imani ninayo kweli, muumba nanyenyekea
Dhambi zangu ziwe mbali, niombapo hili dua
Mola wetu watujali, wema wako twaujua
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Tazama na majambaziwasokuwa na hisani
Waua hata wazazi, na matendo yalo duni
Naomba zako bawazi, tuzingire masihani
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Vita navyo vimechacha, eti kudai mashamba
Makao mengi kuacha, kuwindwa kama simba
Vilio usiku kucha, mateso mengi kupamba
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Zilizala kuhofisha, viwewe tele nyoyoni
Redio zikatupasha, habari zenye makini
Kiini chake Arusha, na kuzagaa nchini
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Magenge yenye mapanga, yahofisha wananchi
Na njama kuzipanga, mchana bado mbichi
Kuvamia na viunga, kutwanga watu michi
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Ukimwi zimwi katili, laua pasi huruma
Hili janga nakubali, halina mtenda wema
Ombi langu kwa jalali, maisha yawe ni mema
Naomba utunusuru, majanga kila pahali.

Nimefikia tamati, nikiwa nayo imani
Tufuateni Torati, amri zake Manani
Atulinde na mauti, au maovu duniani
Naomba utunusuru, majanga kila pahali


Comments about Majanga Yatumaliza by KAPCHANGA MARK KWEMOI

There is no comment submitted by members..Read this poem in other languages

This poem has not been translated into any other language yet.

I would like to translate this poem »

word flags

What do you think this poem is about?Poem Submitted: Wednesday, April 16, 2008[Report Error]