Vukani Poem by Fadhy Mtanga

Vukani

Nasema wote vukani, sauti zisikieni,
Tokeni usingizini, inukeni vitandani,
Tufanye jambo fulani.

Nasema wote vukani, ujasiri onesheni,
Isiwe kama zamani, za utumwa fikirani,
Kwani hiyo ni amani.

Nnasema wote vukani, mbiu kubwa ipigeni,
Isikike milimani, hata huko mabondeni,
Wote wakusikieni.

Nasema wote vukani, jikwamue akilini,
Sisi si mahayawani, twajua twataka nini,
Tungali mapambanoni.

Nasema wote vukani, mama wote majumbani,
Utumwa ukataeni, utumwa wa kizamani,
Imara msimameni.

Nasema wote vukani, nyie daraja la chini,
Kunyonywa kakataeni, maana ni ushetani,
Unyonyaji upingeni.

Nasema wote vukani, wanafunzi mavyuoni,
Ubaguzi ondoeni, ule kwenye udhamini,
Msikubali jamani.

Nasema wote vukani, nyie wa maofisini,
Hujuma zizuieni, ufanisi ujengeni,
Fitina iepukeni.

Nasema wote vukani, ambao mnazo dini,
Kamwe wasiwarubuni, ikapungua imani,
Mkajenga ufitini.

Nasema wote vukani, bado tungali vitani,
Hakuna raha moyoni, bado tungali shidani,
Hebu tujikwamueni.

Nasema wote vukani, tusilale asilani,
Usingizi uacheni, huleta umasikini,
Nieleweni jamani.

Nasema wote vukani, isiwe kama zamani,
Tutalala hadi lini, turidhike mioyoni?
Vukani basi jamani.

Nasema wote VUKANI!

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success