Mbali Nawe! Poem by Fadhy Mtanga

Mbali Nawe!

Jua linapochomoza, kila siku asubuhi,
Hunifanya kukuwaza, unipaye kufurahi,
Maneno ninayokweleza, ni ukweli si kebehi,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

Wewe u sehemu yangu, nuru yangu maishani,
Nilopewa na Mungu, niwe nayo duniani,
Nitayaonja machungu, siku siponithamini,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

Daima uwapo mbali, hata ni kwa siku moja,
Nitakesha mi’ silali, nikeshe nikikungoja,
Tukae sote wawili, tufurahi kwa pamoja,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

Huhisi nina adhabu, napokuwa mbali nawe,
Maisha kunighilibu, nami nichanganyikiwe,
Wewe nd’o wangu muhibu, sina tena mwinginewe.
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

Nakuwa mi’ na upweke, nazo karaha moyoni,
Nayo maji yasishuke, niyanywapo mdomoni,
Yafanya nitaabike, nijawe nayo huzuni,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

Nakosa mie furaha, nakumbwa nao unyonge,
Maisha yawa karaha, kunifanya nisiringe,
Wala sifanyi mzaha, nisemayo siyapinge,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichikipenda.

Sogea kwangu karibu, ee pambo la wangu moyo,
Pendo silolihesabu, amini niyasemayo,
Ya moyo wangu dhahabu, unipaye pasi choyo,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisichokipenda.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success