Kichaa Anena. Poem by Abdallah Mpogole

Kichaa Anena.

Katika hadhara kubwa, watu wameshika tama.
Yatoka sauti kubwa, napenyeza kina mama.
Mara kibao nazabwa, uwi! Uwi mh kichaa!
Pungufu hawezi kuwa, maneno yake yafaa.

Nasonga bavuni kwake, asije nipiga ngumi.
Atamba sie wa kwake, apite mbili na kumi.
Hizo ndo kauli zake, atumeza kwa makumi.
Huyu kichaa jamani, mbona hakosei tungo?

Miguo yake michafu, mbona ndimi zake safi?
Acheka na kusanifu, ahoji nani yu safi.
Kimya! Japo tu nadhifu, aponda walo walafi.
Kichaa ajua nchi, siasa kafunzwa wapi?

Alonga yeye Raisi, mwakani hatotwachia.
Adai kura hakosi, dhalimu hatomwachia.
Taweka kote vikosi, hakuna wa kumwibia.
Kichaa ataka pewe, nchi ya wendawazimu.

Hataki tena fisadi, bora machifu wa jadi.
Wote aita gaidi, wajimegea kuzidi.
Atabiri ya Burundi, tushagawika makundi.
Wamchefua uozo, kichaa wa jalalani?

Tukisita atatoa, kunuka hatotishika.
Halei tena madoa, mchezo wa kuchafuka.
Kwanini twajipodoa, twachukia kuzeeka.
Kichaa maoni yake, tulo timamu twacheka.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success