Najiuliza mie, ntapata kwa vipi kazi.
Mbinuzo mnigawie, nijaribu panda ngazi.
Niteni nkaribie, wasijutie wazazi.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Nalijaribu mavazi, sikumvutia bosi.
Pozi la kimaongezi, katu sikuweza pasi.
Nalisoma nayo kozi, kimombo kinipe kasi.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Ambatisha na vivuli, baruani niliweka.
Sikuitwa usaili, nikatoka tena kapa.
Si moja wala ya pili, ndoto zimeshafutika.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Ya wengi nawakilisha, wahangaikao kucha.
Soli za viatu kwisha, pilika hatwezi acha.
Nabadili tu bahasha, nauli kwisha nachacha.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Kauli mbiu ni kazi, natafuta wajameni.
Nipeni japo uwazi, nipate matumaini.
Kumi nne zangu ngazi, nimepitia shuleni.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Kiswahili yangu lugha, naweza na ushairi.
Kijana mwenye shabaha, ntaandika habari.
Ishirini na sabha, mjamaa wa kadiri.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Rushwa kwangu yu adui, nalifundishwa zamani.
Wote wangu sibagui, chui mtu siamini.
Nadumaa na sikui, si mchana si jioni.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Wino kwenye tamati, sioni palo hakika.
Nimevunja kamati, sijafika muafaka.
Jasho ndo maji ya shati, utuli sasa wanuka.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
Salamu zenu wazazi, mwanenu bado nasaka.
Mie ndo wenu mlinzi, ahadi nazikumbuka.
Tumwombe mola mwenyezi, milango itafunguka.
Ipi njia mulopita, nipitisheni na mie.
This poem has not been translated into any other language yet.
I would like to translate this poem