Naugua Juu Yako Poem by Fadhy Mtanga

Naugua Juu Yako

Naugua juu yako, mwenzio mie nakonda,
Na mawazo juu yako, yanipa vingi vidonda,
Naugua juu yako.

Mawazo wakati wote, mwenzio yaniandama,
Nahitaji nikupate, nitateswa nayo homa,
Naugua juu yako.

Niseme unisikie, mwenzio naugulia,
Ili unifikirie, nami nipone ugua,
Naugua juu yako.

Naumwa mie naumwa, nimepandwa nayo homa,
Nitowe kwenye utumwa, niwe chako chanda chema,
Naugua juu yako.

Maradhi hayatibiki, dakitari wangu wewe,
Uniondolee dhiki, nifanye nisipagawe,
Naugua juu yako.

Upweke unanitesa, nakutamani karibu,
Nilipate penzi hasa, unipe ewe muhibu,
Naugua juu yako.

Uniponye nikapona, nipone jamani mie,
Uniponye nikapona, maradhi 'sijirudie,
Naugua juu yako.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Fadhy Mtanga

Fadhy Mtanga

Dar es Salaam, Tanzania
Close
Error Success