Nimekukumbuka Sana. Poem by Abdallah Mpogole

Nimekukumbuka Sana.

1. Nashindwa kujitambua, ni hali gani nipo.
Siku gani nitapoa, niendako weye upo.
Maishani kwangu doa, sijasahau kiapo.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

2. Nilalapo sikwoti, na pichazo hazifiki.
Weye kwangu ni bahati, u nyota ya Mashariki.
Sintoweza kusaliti, na sifanyi unafiki.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

3. Sitaki kusononeka, kwangu mie kutokwona.
Mwilini naholojeka, ulipo Simu hakuna.
Jikaze watakucheka, Babayo utaniona.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

4. Nasikia u mkubwa, ati dukani waenda.
Huli tena vya kupondwa, ngumi teke waziponda.
Sikuona ukibebwa, ni lini ulipokonda.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

5. Nakumbuka siku zile, natoka kwetu chuoni.
Nilifaidi kelele, tukalala kitandani.
Nikanyoa zako nywele, nikiimba sikioni.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

6. Mie bado ninaishi, usijesikiza watu.
Wapo wengi wa uzushi, sadiki usithubutu.
Watoe nayo matusi, eti sikupi kiatu.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

7. Sikutaka kufikia, haya yote kukwandikia.
Nashindwa kujizuia, omba watakusomea.
Siku tajanijibia, yote nilokwandikia.
Upo kwangu mawazoni, japo sikwoni machoni.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success