Nyerere Baba. Poem by Abdallah Mpogole

Nyerere Baba.

Nisaidieni leso, machozi nijifutie.
Alotabiri ya kesho, hatunaye nikwambie.
Mwalimu wetu spesho, habarize uzijue.
Nyerere namlilia, natamani anisikie.

Alimtoa mkoloni, bendera yetu angani.
Umoja nayo amani, katutoa ujingani.
Kabila kwetu utani, tumesifika barani.
Nyerere katupa lugha, nalonga bara na pwani.

Uongoziwe nchini, tawala bora nadhifu.
Nahodha huyu makini, mpingaji uhalifu.
Alojali masikini, kila kona wamsifu.
Nyerere Baba u' wapi, itika nikusikie.

Ujamaa ulileta, Azimio la Arusha.
Wote kujitegemea, mali wote kututosha.
Kwa pamoja kupangana, hakuna wa kukatisha.
Nyerere nifungulie, yapo mengi nikwambie.

Nimeona niandike, barua hii ifike.
Maisha yangu upweke, nchi yote ni ya kwake.
Nakula yalo mapeke, nyama nzima ala peke.
Nyerere Baba mwambie, wewe ndo akusikie.

Misingi ulotufunza, wachache wamegeuza.
Kunguni wanatufyonza, vitini wamejibanza.
Nchi yazidi kuoza, yatoka nayo mafunza.
Baba ulo taa yetu, nuru ya wanyonge wote.

Nyumbayo sasa kificho, wala bila wasiwasi.
Wajichana pochopocho, wapatiana nafasi.
Watuzika hali macho, kupunguza zetu ghasi.
Nyerere Baba wa kweli, hukutenga wasomali.

Tamati yangu sikia, ni mengi ya kwongeya.
Kwanza mstari pigia, majibuyo nangojeya.
Suluhu pa kuanzia, kwani nazidi umiya.
Nyerere hekima zako, Taifa tukawa sawa.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success