Napenda Kuandika. Poem by Abdallah Mpogole

Napenda Kuandika.

Rating: 3.5

Kalamu ya risasi tosha, naandika na kufuta.
Matendo yalonikosha, pia yalonikokota.
Yote nayaoanisha, wazo kamili napata.
Kwa njia ya ushairi, mie hupenda kuandika.


Lugha yangu ni rahisi, yeyote ataisoma.
Natoa ilo halisi, uwongo waja nichoma.
Hamasa na ufanisi, najifunza toka zama.
Ushairi ulo wazi hujikita kwa jamii.


Nawe naomba usome, kesho ushike kalamu.
Zilo mbivu uzichume, walishe wapate hamu.
Nikosowe nijitume, niithamini kalamu.
Ushairi kwazo beti, tufundishe maadili.


Nyimbo za chekecheani, na hadithi za nyakati.
Pia zao tafrani, za masai na mang’ati.
Sekeseke za mitaani, na mbu funua neti.
Shairi lajazwa ladha, kwa lugha ilo mkato.


Naandika lugha ya watu, Kiswahili ndo chetu.
Nawazima roho kwatu, wanoabudu ya watu.
Haishiki kutu katu, haipambi ukurutu.
Shairi lilo hisia, hakika talirudia.


Wanoumwa subiria, zipo dawa nawagea.
Tamathali ndo tumia, siku zote kwa kwongea.
Hisia sije achia, mafumbo sije tegea.
Shairi liwe makini, lipambwe vina mizani.


Iwe dhiki au nema, sintopotosha asili.
Lilo baya liwe jema, mi si pungufu akili.
Sintochelea kusema, japo meshika makali.
Shairi ni kama tumbo, njaa yake iwe wimbo.


Tamati nina kiburi, lughaye Kiswahili.
Yatamba zote bandari, yauza bila dalali.
Wateja haisubiri, wafata wale asali.
Napenda tena andika, shairi la kusomeka.

COMMENTS OF THE POEM
Michael Walkerjohn 21 October 2014

Aloha Abdallah... Habari, Hujambo? I have surfed over your post just now... I am working on its translation and hope to be more concise in a future response to you... This moment I have my thanks to you for your work... Poetry is a most complicated form of communication... your efforts have my interest... all of the best from this life, to you, and all of your relations... Michaelw1two

0 0 Reply
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success