Ewe Nyota. Poem by Abdallah Mpogole

Ewe Nyota.

Siku nyingi zimepita, tangu ulipoondoka.
Salamu zako napata, wasafiri wakifika.
Upweke wanikong'ota, wapinzani wanicheka.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Nawaza mpaka nagota, ni vipi uliondoka.
U wapi wangu kashata, mdomo wankauka.
Nshalamba nyingi karata, wanimaliza na joka.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Ulinifanya kumeta, ni wapi tusosikika.
Nipewe hata ya bata, cheo chochote Afrika.
Utamuwo sintopata, madhila sintoepuka.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Maradhi yaniandama, matabibu wameshindwa.
Peke yangu ninalalama, mi hayawani natengwa.
Fikra tele nazama, barabarani ntanyundwa.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Jitahidi uje nkuta, japo mkono kunshika.
Sioni pa kukamata, si punde ntadondoka.
Timamu hutonkuta, weledi wazidi ntoka.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Upya wetu tungerudi, ningeliepa kabuli.
Kusubiri sina budi, hatima yangu jalali.
Nilizivunja ahadi, nilizongwa sikujali.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Sikuwa muadilifu, vipusa walinimeza.
Kwayo mengi majisifu, walevi kunipongeza.
Waliniita nadhifu, pindi ninakufukuza.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

Uterezi wanizidi, kalamu yanidondoka.
Moyo wangu u' baridi, nguvuye yapukutika.
SHIHATA muiradidi, habari iweze fika.
Ewe nyota nakuota, lini utanikumbuka.

COMMENTS OF THE POEM
READ THIS POEM IN OTHER LANGUAGES
Abdallah Mpogole

Abdallah Mpogole

Iringa, Tanzania
Close
Error Success